Katibu wa chama cha Knut katika Kaunti ya Mombasa Dan Aloo amepinga kauli ya Waziri wa Elimu nchini Dkt Fred Matiang'i kuwa hakuna upungufu wa walimu nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumatano, Aloo alisema kuwa Kenya inakumbwa na uhaba wa walimu takribani laki 150 ambapo mwalimu mmoja analazimika kuwahudumia zaidi ya wanafunzi 100.

“Nilishangaa sana kumsikia waziri wa elimu akisema kuwa Kenya ina walimu wa kutosha, ilhali ukiingia darasani utapata mwalimu mmoja akihudumia zaidi ya wanafunzi 100 ,kinyume cha sheria inayopendekeza kati ya wanafunzi 30-35 kwa mwalimu mmoja,” alisema Aloo.

Aidha, Aloo alitaja mazingira mabovu ya kusomea na ukosefu wa vifaa muhimu vya masomo kama chanzo cha matokeo duni katika baadhi ya shule nchini.

Alisema kuwa matokeo duni hayasababishi na kuzembea kazini kwa walimu kama alivyodai Matiang’i.

“Tunakuwa wepesi kuwalaumu walimu wakati matokeo yanapokuwa mabaya, lakini tunasahau kuwa hawa walimu hawawezi tekeleza wajibu wao ipasavyo bila mazingira ya masomo kuboreshwa,” aliongeza Aloo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Elimu Fred Matiang'i alikosoa shinikizo zinazotolewa na Knut la kuwaajiri walimu zaidi, kwa kusema kuwa idadi ya walimu iliyoko kwa sasa inatosha kuwahudimia wanafunzi, ila ni utepetevu unaochangia matokeo mabaya.