Share news tips with us here at Hivisasa

Chama cha walimu cha Knut tawi la Nakuru kimewataka walimu kutotia saini mikataba ya utendakazi.

Akitoa wito huo, katibu mpya wa chama hicho tawi la Nakuru James Muhia alisema kuwa walimu hawafai kutia saini mkataba huo hadi majadiliano yafanywe baina yao na serikali.

Ni wito sawia na ule ambao umekuwa ukitolewa na katibu mkuu wa Knut Wilson Sossion ambaye alisema kandarasi hiyo ya utendakazi ni adhabu kutoka kwa mwajiri wao, huku chama hicho pia kikilalama kuwa Tume ya kuwaajiri walimu TSC haikuwahamasisha kuhusu zoezi hilo.

Aidha, Knut imewataka walimu kususia zoezi hilo hadi pale afisi hiyo itakapofahamishwa kuhusiana na swala hilo.

Hii ni licha ya TSC kusisitiza kuwa zoezi la kubuni kandarasi hizo lilihusisha washikadau wote katika sekta ya elimu miongoni mwao wakiwa viongozi wa elimu.

Wakati huo huo, katibu huyo amelalama kuwa serikali inawakandamiza kwa kutowahusisha katika maamuzi maalum yanayofanywa na yanayowalenga.

Muhia alisisitiza kuwa walimu wanafaa kuhusishwa katika maamuzi hayo, ili sekta ya elimu iweze kuboreshwa.

Akiangazia matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE, yaliyotolewa siku ya Alhamisi, Muhia ameitaka serikali kupitia kwa wizara ya elimu kutumia matokeo hayo kubaini kuwa walimu wana uwezo wa kuboresha elimu.