Aliyekuwa mbunge wa Subukia Koigi Wa Wamwere, amempongeza waziri wa elimu nchini Fred Matiang’I kufuatia hatua yake ya kuvunjilia mbali baraza la mitihani nchini knec na kuwachukulia hatua za kisheria maafisa wa baraza hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza mjini Nakuru siku ya Jumamosi, Bw Koigi alisema hatua ya matiangi ni ya kijasiri lakini akashikilia kuwa alichelewa katika kufanya uamuzi huo.

Alisema maswala ya udanganyifu katika mitihani ya kitahifa yalitokana na maafisa hao kujihusisha na ufisadi kwa njia moja au nyingine katika baraza hilo.

"Japo Matiangi amefanya jambo la Busara, kwa maoni yangu nafikiri hatua hii angechukua punde tu baada ya kuripotiwa wizi wa mitihani lakini hata hivyo nampongeza kufuatia hatua aliyoichukua,” alisema Koigi.

Bodi ya baraza la mitihani ya kitaifa ya KNEC ilivunjiliwa mbali huku waziri wa elimu Fred Matiang’i akisema alichukua hatua hiyo kama moja wapo ya mabadiliko yanayofanywa katika sekta ya elimu na haswa uongozi wa mitihani ya kitaifa.

Matiang’i alimteuwa Prof George Magoha kuwa mwenyekiti mpya wa bodi hiyo.

Pia alitoa agizo la kukamatwa na kuandikisha taarifa mara moja kwa aliyekuwa mwenyekiti Joseph Kivilu na maafisa wakuu kuhusu viwango vya juu vya wizi wa mtihani ulioshuhudiwa mwaka jana.