Aliyekuwa mbunge wa Subukia Koigi wa Wamwere, amesema kuwa hotuba aliyotoa naibu wa rais William Ruto siku ya Jumanne kuhusu hali ya taifa, ilikuwa ni kuisifu serikali ya Jubilee pekee kwa kuwa hakuangazia baadhi ya ahadi ambazo haijatimiza pamoja na changamoto wanazozipata wanapojaribu kuzitekeleza.
“Nilitarajia kuwa naibu wa rais angezungumzia mafanikio pamoja na changamoto za serikali lakini alizungumzia ilikofaulu pekee na kuacha yale ambayo haijatimiza, kwa maoni yangu alikuwa anaisifu Jubilee tu.” Alisema Koigi.
Akizungumza katika kipindi cha kituo cha redio cha Sauti ya Mwananchi mjini Nakuru Jumatano, Koigi alisema vile vile hakuridhika na jinsi naibu wa rais alivyoangazia swala la ufisadi katika hotuba yake, huku akisikitika kwa hatua ya naibu wa rais kutozungumzia swala la ukabila ambalo hata alikuguziwa na naibu wa rais katika hotuba hiyo.
“Nilisikitika sana nilipogundua kuwa naibu wa rais hakuliguzia hata kidogo swala la ukabila ambalo ndilo linalosababisha taifa hili kukumbwa na maovu mengi,” Koigi alisema.
Ameitaka serikali kutohepa maswala nyeti kama ukabila na ufisadi, ambayo yanawakumba wananchi na taifa kwa jumla na badala yake kuyachukulia kwa uzito na kuyaangazia kwa upana na marefu.