Kiongozi wa Chama Cha Mwananchi Koigi wa Wamwere amesema majaaliwa atajibwaga kwenye kinyang’anyiro cha kutwaa kiti cha useneta kaunti ya Nakuru mwaka wa 2017.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Siku ya jumanne, Koigi alishikilia kuwa ana rekodi nzuri ya maendeleo.

Koigi alisema kwamba siasa za Nakuru zinahitaji mabadiliko makubwa ya uongozi na maendeleo kwani gavana wa sasa Kinuthia Mbugua na seneta James Mungai, kwa pamoja "wamewafeli wakaazi wa kaunti hiyo kwa kutoleta maendeleo yoyote yanayoonekana”.

“Seneta Mungai ndiye amefeli wakaazi wa Nakuru hata zaidi. Hafuatilii pesa zinavyotumika katika kaunti, yeye amefeli hata kuliko gavana,” Koigi aliongezea.

“Mungu akipenda nitajibwaga kwa sababu naamini ile kazi ya seneta ambayo nitaomba nitaweza kuifanya vyema kuliko wengine ambao wamejitokeza kuomba kiti hicho” Koigi akasema akizungumza katika kongamano moja la mataifa ya Kenya na Venezuela jijini Nairobi Jumanne.

Mwanasiasa huyo alisema rekodi yake inajieleza yenyewe kuhusiana na aliyofanya wakati akiwa mbunge.

“Nimefanya vizuri katika siasa. Nimesaidia kuleta uhuru wa pili katika nchi hii, nilipeleka miswaada ya kusaidia watu kupunguziwa kodi bungeni, nilisimamia CDF ya Subukia vizuri na kufanya miradi hadi ikawa mfano. Nilisaidia kupelekea watu wa Subukia chakula wakati walikuwa na njaa. Kwa hivyo ninaweza kusema kwamba kama nimefanya vizuri, ninastahili kupewa nafasi tena kuendeleza watu wa kaunti ya Nakuru,” alisema Koigi.