Viongozi mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria kongamano la kutafuta suluhu la mgogoro baina ya wanyama na binadamu litakaloandaliwa hapo kesho katika hoteli ya Voi safari lodge katika kaunti ya Taita Taveta.
Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na serikali kuu kupitia serikali ya kaunti ya Taita Taveta ikishirikiana na wizara ya mazingira, raslimali asili na mamlaka ya maendeleo pamoja na shirika la huduma kwa wanyama na tume ya kitaifa ya uwiano na maridhiano NCIC inapania kuandaa kongamano hilo ambapo viongozi wa serikali kuu pamoja na za kauti watazungumzia namna ya kukabiliana na vita vya mara kwa mara baina ya wanyama na wakazi wa eneo hilo.
Mgogoro baina ya wanyama pori na wananchi hapa nchini umezidi kushuhudiwa katika kaunti mbalimbali huku wakazi wa Pwani haswa wanaoishi karibu na mbuga za wanyama kama vile mbuga ya wanyama ya shimba hills ambao hukadiria hasara kila wakati kwa kuharibiwa mazao yao shambani huku wale wa Taita Taveta wakihangaishwa na wanyama hao ambao kila mara wanaonekana kukumbana nao katika shuhuli zao za maisha na hata kuwaweka katika hatari.
Aidha watakaohudhuria kongamano hilo ni pamoja na waziri wa mazingira profesa Judy Wakhungu, katibu mkuu katika idara ya mazingira Magret Mwakima, mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya uwiano na utangamano Francis Ole Kaparo, Mkurugenzi mkuu wa shirika la huduma kwa wanyama pori na seneta wa Mombasa Hassan Omar miongoni mwa viongozi wengine.
Kongamano hilo ambalo litachukua siku moja linatarajia kutoa suluhu ama mwelekeo wa namna wananchi watakavyotangamana na wanyama pasi kuathirika.