Share news tips with us here at Hivisasa

Askofu wa kanisa la katoliki dayosisi ya Eldoret Cornelius Korir amesema visa vya wizi wa mifugo katika maeneo ya Bonde la Ufa vimerudi chini.

Askofu Korir alisema visa hivyo vimerudi chini kutokana na juhudi za wadau mbali mbali kushirikiana katika harakati za kuhubiri amani na upatanisho miongoni mwa jamii ambazo zimekuwa na changamoto ya wizi huo.

“Ukweli ni kwamba visa vya wizi wa mifugo na utepetevu wa amani kwa jumla vimerudi chini katika eneo hili, tunashukuru Mungu kwa sababu wananchi wametusikiza kama kanisa na kukubali kuachana na tamaduni ya wizi wa mifugo,” alisema Korir.

Akihutubu mjini Eldoret Jumatatu, Korir alisema kanisa lake kwa ushirikiano na wadau wengine inashirikiana na mabaraza ya wazee ili kubuni kamati zaidi za amani na upatanisho mashinani.

Kwa mujibu wa askofu Korir, kamati hizo zitabuniwa katika kila kijiji ili kufikia wananchi mashinani na uhamasisho kuhusu umuhimu wa kudumisha amani.

“Tunalenga kushirikiana na mabaraza ya wazee kutoka katika jamii zote za Bonde la Ufa ili kubuni kamati za amani na upatanisho mashinani kwa ajili ya kudumisha amani ambayo tunashuhudia kwa sasa, hasa katika maeneo ambako wizi wa mifugo ulikuwa umekita mizizi,” alisema Korir.

Askofu Korir alitaka wanasiasa kujiepusha na tabia ya kugawanya wananchi kwa misingi ya kikabila wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi huyo alitahadharisha wanasiasa dhidi ya kutumia changamoto ya kesi dhidi ya naibu rais William Ruto na mwana habari Joshua Sang kujitafutia makuu kisiasa.

"Si vyema kwa wanasiasa kutumia swala la ICC kujipendekeza katika jamii fulani kwa kujifanya wana ushahidi kuhusu waliomsababisha Ruto masaibu ya kuwa katika mahakama ya ICC,” aliongeza.