Timu ya halmashauri ya Bandari katika mchezo wa vikapu kwa wanaume itafungua kampeni za kuwinda ubingwa wa ligi kuu ya vikapu nchini na mechi dhidi ya timu ya Co-operative Bank Spartans siku ya Jumapili.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baada ya kukosa kushiriki mkondo wa kwanza wa ligi hiyo wikendi iliyopita kutokana na sababu ambazo zilitajwa kama ambazo hazingeweza kuepukika, Bandari chini ya kocha Anthony Ojukwu italazimika kuwa katika viwango ubora ili kuwapiki Spartans ambao ni mabingwa wa zamani.

Bandari ilipoteza ubingwa wake kwa timu ya wanajeshi ya Ulinzi Warriors msimu uliopita lakini kocha Ojukwu ameeleza imani yake kuwa vijana wake tayari wameyarekebisha mapungufu waliyokuwa nayo msimu jana na sasa wakao tayari kuhakikisha kuwa wanalitwaa taji kuu msimu huu.

Kwenye mazungumzo kwa njia ya simu na mwandishi huyu mapema siku ya Ijumaa kabla ya kufunga safari ya kwenda Nairobi, Ojukwu alisema kuwa anautambua upinzani uliopo kwenye ligi lakini timu yake ina makali ya kutosha ya kuukabili ushindani huo.

‘’Kikosi kiko sawa, tuko tarayi na tutajituma zaidi ili tulilete taji Mombasa. Makosa tuliyoyafanya msimu jana tayari nimeyarekebisha sasa ni wakati wa kuzoa ushindi,’’ alisema Ojukwu.

Mechi hiyo itachezwa katika ukumbi wa Nyayo siku ya Jumapili.