Halmashauri ya bandari nchini KPA, imesema haitaruhusu meli za mafuta kutia nanga bandarini humo wakati wa usiku, kama njia moja ya kuzingatia masuala ya usalama.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mkuu wa huduma za baharini, William Ruto, ameeleza kuwa kuruhusu huduma za mafuta kufanywa wakati wa usiku itagharimu KPA fedha nyingi.

Akizungumza siku ya Jumanne kwenye warsha iliyowajumuisha maafisa kutoka KPA na wadau katika sekta ya mafuta kwenye hoteli moja mjini Mombasa, Ruto alisema hakuna haja ya kupunguza muda ambao meli hutumia kupakua mizigo.

Wakati huo huo, mkurugenzi mkuu wa KPA Catherine Wairi ambae aliwakilishwa kwenye warsha hiyo na mhandisi Abdullahi Samatar, alieleza kuwa mwaka jana KPA ilisimamia tani milioni 26 za mizigo ambapo asilimia 27.2 kati yake ilikuwa ni aina tofauti za bidhaa za mafuta.

Wairi alisema kuwa KPA kwa sasa iko kwenye mchakato wa kubadilisha eneo la kuegesha shehena za mafuta la Kipevu Oil Terminal, ili kufikia mahitaji ya Wakenya ambapo eneo hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya mapipa elfu 200 ya mafuta.