Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Bandari nchini KPA, Catherine Wairi amewaonya wadau mbalimbali wa kibiashara wanaotumia Bandari ya Mombasa kujiepusha na sakata za ufisadi.
Kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya Halmashauri hiyo mjini Mombasa siku ya Jumatano, Wairi alisema kuwa halmashauri hiyo haiwezi kuruhusu ufisadi kufanyika katika bandari hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa watakaopatikana watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha, alisema kuwa halmashauri hiyo iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali wa kibiashara ambao wako tayari kupiga vita ufisadi katika bandari hiyo, ili kuhakikisha kuwa shughuli za kibaishara zinafanyika vyema,
Wairi alisema kuwa bandari hiyo inatumika na nchi nyingi za Afrika hivyo basi lazima shughuli zake kuwa wazi.
"Kama viongozi wa KPA, kamwe hatuawezi kukubali kuendelea kushuhudiwa kwa sakata za ufisadi bandarini. Yeyote atakayepatikana akishiriki ufisadi iwe wa kutoka sekta za biashara za umma ama binafsi, lazima atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Wairi.
Wakati huo huo, mkurugenzi huyo aliahidi kuimarisha mazingira ya wafanyikazi huku akisema kuwa swala la ukabila na siasa katika usimamizi wa bandari hiyo umepigwa marufuku, na lazima kila shughuli za uajiri na utaoji zabuni kufanyika katika njia ya uwazi na haki.