Afisa mkuu mtendaji wa Tume ya maadili na ufisadi EACC, amesema kuwa zaidi ya visa 300 vya ufisadi vinavyokabili Halmashauri ya Bandari nchini KPA, vimeripotiwa katika afisi yake.
Akizungumza jijini Mombasa siku ya Jumapili katika kongamano lililoandaliwa na KPA na Tume ya EACC, Halakhe Waqo alisema miongoni mwa visa hivyo ni kupotea kwa makasha katika Bandari ya Mombasa.
Waqo alisema kuwa bado uchunguzi unaendelea kuhusu ripoti hizo za ufisadi na kusisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
“Bado uchunguzi wa ripoti hizo unaendelea na tutahakikisha waliohusika wanakabiliwa kisheria,” alisema Waqo.
Waqo alisema kuwa tayari watu 14 wamefunguliwa mashtaka.
Aidha, Waqo amependekeza kuongezwa kwa sehemu za kukagua makasha ili kuziba mianya ya kukwepa ushuru na mali kuibiwa.