Share news tips with us here at Hivisasa

Hatimaye muungano wa KPAWU umeanzisha misururu ya uchaguzi wa kuwachagua makatibu wa muungano huo kwenye matawi yake kote nchini.

Akihutubu kwenye uwanja wa Shule ya msingi ya Sotik Highlands baada ya uchaguzi wa maafisa wa chama hicho tawi hilo kukamilika siku ya Jumamosi, katibu mratibu wa kitaifa wa chama hicho Henry Omasire, alisema sharti viongozi walioteuliwa washirikiane kuhakikisha maslahi ya wanachama yanaangaziwa hasa kwa kuhakikisha mashine za kuchuna chai haziruhusiwi kuchukua nafasi za wafanyikazi.

"Viongozi mliochaguliwa sharti mshirikiane kuhakikisha kuwa maslahi ya wafanyikazi wote yanaangaziwa. Sharti muweke mikakati ya kusitisha utumizi wa asilimia kubwa ya mashine zinazochuna chai kwa kuwa zimechukua nafasi kubwa ya wafanyikazi," alisema Omasire.

Katibu huyo aidha alisuta watu wanaopinga kuchaguliwa kwa viongozi wa tawi hilo, akihoji kuwa mpinzani wa katibu wa eneo hilo hakuwa ametuma maombi ya kutaka kuwania cheo hicho, hali ambayo imesababisha katibu wa zamani Stephen Nyamweno kuteuliwa moja kwa moja.

"Haya mambo ya baadhi ya watu kusema kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki ni porojo tu zisizo na msingi. Katibu amechaguliwa moja kwa moja kwa sababu ya kutokuwepo na mpinzani," alisema Omasire.

Charles Yuvinalis Kegicha alichaguliwa mwenyekiti wa muungano huo, huku Stephen Nyamweno akichaguliwa kama Katibu na Josiah Kayo kama mwekahazina.