Shirika la ukusanyaji ushuru nchini KRA limesema kuwa liko tayari kusuluhisha mzozo kuhusu ushuru baina yake na kampuni inayotengeza pombe ya Keroche.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kamishna generali wa KRA John Njiraini amesema yuko tayari kuhakikisha kuwa mgogoro ulioko umesuluhishwa haraka iwezekanavyo.

Huku akiwaongoza maafisa wakuu wa KRA katika kutembelea kiwanda hicho mjini Naivasha, Njiraini alisema kuwa wamebuni njia mpya za kuhakikisha wakenya wanafahamu ikiwa bidhaa wanazonunua ni halali.

"Kifaa kipya kitakachowawezesha wakenya kufahamu bidhaa wanayonunua kama ni halali ama ghushi kupitia Smartphone kitaanza kutumika, na kitawasaidia wakenya kwa kiasi kikubwa,” alisema Njiraini.

Kwa mujibu wa afisa huyo, kifaa hicho kinachotumia teknolojia ya kisasa kitawezesha pia kukusanya ushuru zaidi.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Keroche Tabitha Karanja amesema kuwa kifaa hicho kitawawezesha kupigana na pombe haramu zilizo sokoni.

“Tumekuwa tukigongana hapa na pale na KRA, lakini sasa tunashirikiana katika kutimiza matakwa yote yanayohitajika,” alisema Karanja.