Halmshauri ya ukusanyaji ushuru nchini KRA imefanya mnada wa magari ambayo hayajalipiwa ushuru kwa zaidi ya miezi sita katika Bandari ya Mombasa.
Meneja wa mawasiliano katika halmashauri hiyo John Bisonga amesema walichukua hatua hiyo baada ya kuwapatia wenye magari hayo muda wa kutosha kulipa ushuru, ila wakakosa kuitikia wito huo.
Akizungumza siku ya Jumanne wakati wa shughuli hiyo kwenye Bandari ya Mombasa, Bisonga alisema mnada ndiyo njia pekee ya kukusanya ushuru kutoka magari hayo.
Hata hivyo, baadhi ya wanunuzi na wafanyibiashara ambao walijitokeza kununua magari hayo, walipigwa na butwaa kupata bei hazikuwa rahisi kama walivyokusudia.
Hussein Madwan, aliyefika kununua gari aina ya Toyota Belta alilalamikia bei ya gari hilo iliyokuwa ikiuzwa kwa shilingi milioni moja ikilinganishwa na bei ya kati ya shilingi laki saba hadi nane katika yadi za kuuza magari.
Kwa upande wake, Meshack Owino ambaye hushiriki sana katika mnada wa KRA vile vile alieleza kutoridhishwa kwake na bei hizo za juu, na kusema kuwa alishangazwa na jinsi watu wengine walivyojitolea kununua magari hayo.