Mamlaka ya ushuru nchini KRA inazuilia magari mawili aina ya Range Rover na Mercedes Benz zenye thamani ya shilingi milioni 28 yanazodaiwa kusafirishwa humu nchini kwa njia ya magendo na kupatika katika bandari ya Mombasa.
Kamishna anayesimamia shughuli za mamlaka hiyo katika maeneo ya mipakani humu nchini Julius Musyoki amesema kuwa magari hayo yalikuwa yamefunikwa kwenye kasha la kubeba magodoro na vitu vya kuchekea watoto ili kukwepa kulipa ushuru wa shilingi milioni 8.5.
Akizungumza na wanahabari katika bandari ya Mombasa siku ya Jumanne, baada ya kukagua kasha hilo, Musyoki amesema kuwa kasha hilo la urefu wa futi 40 nambari ya usajili MRKU 202481 kutoka nchini Uingereza mali ya Abubakari Sekimwanyi aliyetambulika kuwa raia wa Uganda itaendelea kuzuiliwa.
Kamishna huyo amedai kuwa maafisa wa upelelezi, wale wa KRA na KPA wanashirikiana kuchunguza makasha mengine zaidi ili kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinazoingizwa katika bandari ya Mombasa kwa njia ya magendo zinakamatwa na wahusisha kuchukuliwa hatua za kisheria.
"Maafisa wa KRA, KPA na wale wa upelelezi wanaendelea kuchunguza maksha mengine katika bandari hii na tunaimani kuwa tutanasa makasha mengine hadi tuona kuwa maswala ya uingiza na usafirishaji wa bidhaa za mageni inasitishwa na wafanyibiashara wanalipa ushuru," alisema Musyoki.
Imetoa onyo kali kwa wanaosafirisha au kuingiza bidhaa za magendo nchini kwa kupitia bandari ya Mombasa kuwa watakabiliwa na hata kufungiwa kampuni zao kwa kuhujumu sheria za nchi sawa na kukwepa kulipa ushuru.