Mkuu wa Idara ya kilimo katika Kaunti ya Kisii Vincent Sagwe ameiomba shirika la KTDA ambalo huwasimamia wakulima wa majani chai kuandikisha wakulima hao kwa njia ya teknologia ya kisasa ili kuondoa wakulima bandia.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanamiliki hisa za majani chai lakini sio wakulima halisi wa majani chai hayo, na hupima majani chai kila wakati baada ya kuibiwa kilo za wakulima wengine.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika mji wa Kisii, Sagwe aliwataka wasimamizi wa shirika la KTDA kutembelea kila mkulima na kuwasajilisha kwa teknologia ya kisasa ili kuwaondoa wale ambao si wakulima halisi.
“Kuna watu ambao hujifanya kuwa wakulima wa mmea wa majani chai katika vituo mbalimbali vya kupima majani chai na mara nyingi hupima kilo kwa vituo vya kupima majani chai hayo na si wakulima halisi. Jambo hilo limeleta hasara kwa wakulima wa majani chai katika sehemu mbalimbali hapa kisii,” alisema Sagwe.
Aliongeza, “Naomba wasimamizi wa chama hicho kutembea kwa kila mkulima na kuwasajiri kwa njia ya technologia ya kisaaa ili tuwaondoe wale wanajifanya wakulima wa mmea huo ambao bado wanamiliki hisa nyingi.”
Wakati huo huo ,wakulima wa majani chai kutoka wilayani Gucha wakiongozwa na mwenyekiti wao Peter Momanyi wamelalamikia pesa za ziada ambazo wanakabidhiwa kwa kila kilo.
Wakulima hao walisema hiyo ni hasara kwao na kuna ufisadi unaofanyika kwa uuzaji wa majani chai yao.