Mkurugenzi mkuu wa Chama cha Watalii nchini (Kenya Coast Tourist Association), amesema kuimarika kwa hali ya usalama katika ukanda wa Pwani kwa kiwango kikubwa kumeipiga jeki sekta ya utalii katika eneo hilo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Milicent Odhiambo alisema kuwa juhudi za idara ya polisi kuimarisha usalama humu nchini zimechangia pakubwa katika ukuaji wa sekta hiyo.
Odhiambo alisema kuwa ana matumaini kwamba ukanda wa Pwani utapata watalii baada ya hakikisho kuwa usalama umeimarishwa katika eneo hilo.
Aidha, mkurugenzi huyo alihimiza ushirikiano kati ya Idara ya usalama, serikali na wadau katika sekta ya utalii nchini ili kuiinua sekta hiyo zaidi.
"Sisi kama wadau wa sekta ya utalii tuko na matumaini makubwa kuwa sekta hii itazidi kuimarika kwa kuwa idara ya usalama imetoa hakikisho kuwa Ukanda wa pwani uko salama. Maafisa wa polisi waka macho kuhakikisha kuwa wageni wanaokuja Pwani wako salama, na sisi tunasema kuwa tuko tayari kushirikiana nao ili kuimarisha sekta hii zaidi.” alisema Odhiambo.
Kauli ya Bi Odhiambo inajiri siku chache baada ya Kenya kupokea tuzo kadhaa za kitalii katika hafla iliyoandaliwa mjini Zanzibar, ambapo Mombasa iliorodheshwa kama Jiji linalopendwa zaidi na watali ulimwenguni.
Eneo la Diani lilitajwa kama eneo linaloweza kuwa kivutio kikubwa mno cha watalii katika miaka ya usoni.