Huku taifa likitarajia kujumuika Nakuru Jumamosi kwa maombi ya shukrani baada ya kesi za ICC kutupiliwa mbali, mwanasiasa Stanley Chege Karanja amesema kuwa kuna mengi ya kuafikiwa. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Katika mahojiano Jumapili usiku kwenye Runinga ya K24, Karanja alisema kuwa bado kuna umuhimu wa wananchi kutambua kwamba katiba imewapa nguvu.

Alidai kwamba baadhi ya wanasiasa hawajaamini kwamba kuna mabadiliko ya nyakati, na ni jukumu la mwananchi kuhakikisha uongozi bora. 

"Wananchi wameerevuka na sasa wanafaa kufanya maamuzi bora katika kuwachagua viongozi wenye maono," alisema Karanja. 

Wakati huo huo, alitoa wito kwa taasisi za kikatiba kupewa nguvu zaidi ili kuhakikisha mfumo bora, na kuongeza kuwa taasisi za kikatiba kama vile Mahakama, IEBC na taaisisi ya Rais hazifai kuingizwa siasa. 

"Tunafaa kuzipa nguvu taasisi za kikatiba ili tunapoelekea uchaguzi mkuu ujao pawe na uwajibikaji," aliongeza Karanja. 

Kuhusu swala la ufisadi, Karanja alisema kuwa taasisi ya kupambana na ufisadi humu nchini inafaa kupewa nguvu za kuwatia mbaroni na kuwafungulia mashtaka wale wote wanaopatikana kuhusika na ufisadi. 

Karanja ametangaza azma ya kuwania kiti cha eneo bunge la Nakuru mjini mashariki katika uchaguzi mkuu ujao.