Hali ya wasiwasi imelikumba eneo la Changamwe baada ya kudaiwa kuwa kuna kundi moja la watu linazunguka katika maeneo ya makaazi na kusajili nambari za vitambulisho na kadi za kura kutoka kwa wakaazi bila ya sababu msingi.
Akiyafichua hayo katika kikao na wakaazi wa eneo hilo kilichofanyika katika eneo la Magongo huko Changamwe mjini Mombasa siku ya Jumamosi, mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi amesema kuwa hiyo ni njama ya kuwazuia wakazi hao wasipige kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Mwinyi amedai kuwa ni kupitia kwa njama kama hizo ndipo serikali imekuwa ikiwaibia wakaazi kura hata kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa.
Amewataka wakaazi kuwa makini mno na kamwe kutokubali kusajiliwa nambari zao za vitambulisho au kadi za kura bila ya sababu mwafaka.
“Tunawaomba wakaazi wasikubadili kuwahadaiwa na kufanya uamuzi wa busara kwani kuna njama ya uwizi wa kura kabla ya uchaguzi,” alisema Mwinyi.
Mbunge huyo ameitaka serikali kuweka wazi sababu za kuwasajili wakaazi hao na iwapo ni kisingizio cha kuukabili umaskini basi ni sharti viongozi wa eneo hilo wahusishwe.