Wanafunzi wanaosomea taaluma mbalimbali kwenye vyuo vikuu ambao wanatoka katika familia maskini wamepata sababu yakutabasamu baada ya kikundi cha kina mama wajane kutoka eneo la Mogusii kujitolea kufadhili masomo yao.
Kulingana na msimamizi wa kikundi hicho Helen Aminga, kikundi hicho cha kina mama kina nia yakufadhili masomo ya watoto werevu wanaotoka kwenye familia maskini, wanaosomea vyuo mbalimbali nchini.
"Kama kikundi tuna furaha kwasababu watoto pamoja na jamaa zetu wameweza kuimarika kimasomo kwa hisani ya kundi hili. Kutokana na biashara zetu za kilimo na kama njia mojawapo yakurudisha shukrani kwa jamii, kundi hili lina nia yakuwapa ufadhili watoto mayatima wanaosomea vyuo mbalimbali nchini," alisema Aminga.
Aminga aliongeza kwa kusema kuwa kikundi hicho kina nia yakuwasajili kina mama wengi bila yakujali iwapo wameoleka au la ili kuwasaidia kuafikia matakwa yao kwenye sekta ya elimu.
"Agenda yetu kuu ilikuwa yakuwasomesha watoto wetu lakini sasa kikundi hiki hakitajulikana kuwa cha wajane tu kwa kuwa tuna nia yakusajili kina mama zaidi kwa kuwa tunataka kuimarisha sekta ya elimu hata zaidi," alisema Aminga.
Bi Aminga alisema kuwa kikundi chake kitangoja hadi pale matokeo ya kitaifa ya kidato cha nne yatakapo tangazwa ndipo wajue ni kina nani watakao pata ufadhili huo.
"Tunangojea matokeo ya mtihani wa kitaifa ili kujua ni kina nani watakao hitaji usaidizi wetu. Tunaamini kurudisha shukrani katika jamii, na tunaweza tekeleza hayo kupitia ufadhili kutoka kwa ukulima wetu na kutoka kwa wahisani,” alisema Aminga.