Kundi la akina mama wajane wanaoshughulika na kukausha mboga kutoka kaunti ya Nyamira, watatembea kutoka Nyamira hadi Nairobi kushiriki katika hafla ya maonyesho yatakayofanyika katika jumba la mikutano la KICC.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana kiongozi wa kundi hilo maarufu Nyamira Borabu food processing group, Margret Ombuna, walifikia uamuzi huo baada ya matarajio ya kusaidiwa na serikali ya kaunti ya Nyamira kugonga mwamba.

Kundi hilo liliteuliwa kuuwakilisha mkoa wa Nyanza katika hafla ya kuonyesha tamaduni na ukaushaji wa mboga, ambapo kulingana na Bi. Ombuna, walihitajika shilingi milioni moja kufanikisha safari yao.

Aidha, ameiuliza serikali ya kaunti hiyo kuwasaidia na gari ya Ambulance watakapokuwa wanatembea, ili kuwahudumia watakaolemewa na safari.

“Tulifanikiwa kuchaguliwa kuuwakilisha mkoa wa Nyanza katika hafla hiyo itakayofanyika mjini Nairobi mwezi wa tano. Tunahitajika kuwa na shilingi milioni moja ili kufanikisha safari yetu, lakini matumaini ya kusaidiwa na serikali ya kaunti ya Nyamira haikufanikiwa baada ya kutuambia haina pesa, ambayo imetupelekea kuamua kutembea kwa mguu,” alisema kiongozi huyo.

Aliongeza, “Tunaiomba serikali ya kaunti yetu itusaidie na gari ya Ambulance ili imusaidie atakayelemewa safarini

 Waziri wa biashara Jones Omwenga alisema kuwa serikali ya kaunti ya Nyamira haitakuwa na fedha za kuwasaidia wajane hao.

“Tumekuwa tukiwasaidia akinamama hao lakini kwa sababu bajeti haijasomwa hatutaweza kufadhili safari yao,” alisema waziri Omwenga.