Wakaazi katika mtaa wa Kaptembwa viungani mwa mji wa Nakuru wameteta kutokana na kukithiri kwa kunguni katika makaazi yao.
Wakaazi hao Alhamisi walinena kuwa wanapitia hali ngumu kutokana na kuenea kwa wadudu hao hatari.
"Hali si hali humu.Hatuna amani kwa kuwa kunguni zimejaa kwa nyumba zetu.Tumejaribu kuwaangamiza lakini hawamaliziki kamwe.Tunaomba serikali ya kaunti iingilie kati," alisema Robert Makokha, mmoja wa wakaazi hao.
Maoni hayo yaliungwa mkono na Tabitha Omwenga aliyedai kwamba wadudu hao wamepiga kambi hadi kwa kuta zao hali inayochangia kukithiri kwao.
Aidha hali hiyo imezua hali ya kulauminiana baina ya wakaazi hao wa Kaptembwa na majirani wao wa Rhonda ambao wanawalaumu kwa kuwaeneza wadudu hao madai wakaazi wa Rhonda wamepuuzilia mbali.
"Hawa wadudu chimbuko lao ni Rhonda.Wao ndo wametuletea hii balaa yote kwa kuzieneza kila wanapotutembelea humu mwetu," alisema Martin Gicinga.