Katibu mkuu wa muungano wa walimu nchini Knut Wilson Sossion amesema kuongezwa kwa muda wa masomo katika shule za umma ndio chanzo cha migomo ya wanafunzi inayoshuhudiwa katika baadhi ya shule nchini.
Akizungumza kwenye kikao na waandishi wa habari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Sossion alisema hatua ya Waziri wa Elimu Fred Matiang’i kupiga marufuku likizo fupi ya muhula wa tatu itawanyima wanafunzi nafasi ya kupumzika hasa baada ya kutumia muda mwingi shuleni wataki wa masomo ya muhula wa pili.
“Wanafunzi wanahitaji muda kupumzika baada ya masomo. Waziri Matiang’i angejadiliana na wadau wa sekta ya elimu na hata kuchukua maoni ya wanafunzi kabla kuafikia uamuzi huo,” alisema Sossion.
Aidha, Sossion amesema kuwa kupiga marufuku hafla ya maombi pamoja na kuwazuia wazazi kutowatembelea wanao shuleni wakati wa masomo ya muhula wa watatu hakutasaidia kupunguza visa vya wizi wa mtihani.
“Mtihani hauibwi wakati wa maombi shuleni wala wakati wazazi wanapozuru shuleni kuwatembelea wanao. Mtihani unaibwa katika baraza la mtihani na wale wanaoulinda mtihani wenyewe,” aliongeza Sossion.
Mapema mwezi Aprili, Waziri wa Elimu Fred Matiang’i alitangaza kuongeza masomo ya muhula wa watatu kwa wiki moja zaidi na kufutilia mbali maombi ya kila mwaka wanaofanyiwa watahiniwa kabla kufanya mtihani.