Muungano wa walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri Kuppet, umekosoa Tume ya huduma kwa walimu TSC, kwa kuwalazimu walimu kusalia shuleni wakati wa mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne KCSE na darasa la nane KCPE.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, katibu wa Kuppet tawi la Mombasa, Lynnet Kamadi, ametaja hatua hiyo kama ukandamizaji wa walimu ikizingataiwa kuwa shule za umma tayari zitakuwa zimefungwa kwa likizo ya muhula wa tatu.

“Nadhani TSC inajaribu kutumia mamalaka yake vibaya, walimu wanalazimishwa kusalia shuleni ili wafanye nini? Hii ni kupotezea watu muda. Kama wafanyakazi wengine wa umma walimu pia wanafaa kupewa nafasi ya kupumzika,” alisema Kamadi.

Kulingana na Kamadi, walimu watakaosimamia mitihani hiyo ndio wanaofaa kuwa shuleni badala ya kuwashurutisha walimu wengine ambao tayari kwa muda huo watakuwa wametimiza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Kauli ya Kamadi inajiri siku moja tu baada ya mwenyekiti wa chama cha kutetea maslahi ya walimu Knutt Wilson Sossion kukashifu msimamo huo wa TSC, alioutaja kama unaolenga kuwazuia walimu kujishughulisha na masuala yao kibinafsi wakati wa likizo.

Shule za umma zinatarajiwa kufungwa tarehe Oktoba 28 ili kutoa nafasi kwa mitihani ya KCSE na KCPE.