Chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya kadiri Kuppet kinasema kuwa kinaunga mkono utaratibu wa kuoredhesha shule wakati wa kutangaza mtihani kama ilivyopitishwa na bunge la taifa mapema wiki hii.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Ijumaa, katibu wa Kuppet tawi la Mombasa Lynnet Kamadi alisema utaratibu huo unachangia kuimarisha viwango vya masomo kwa kuwa unaleta ushindani baina ya wanafunzi na shule mbalimbali.

‘’Kuoredheshwa kwa shule kulingana na walivyofanya katika mtihani kunaleta ushindani miongoni mwa wanafunzi. Ushindani huo unawafanya wanafunzi waliokosa kuandikisha matokeo bora kujituma kwenye masomo na hivyo kuimarisha masomo yao,’’ alisema Lynnet.

Hata hivyo, Kamadi anasema Kuppet inapendekeza kando na masomo ya vitabu wanafunzi waorodheshwe kulingana na talanta zao, uwezo wao binafsi na mazingira yao ya masomo.

‘’Nadhani ni jambo lisilo la haki kuwapuuzilia mbali wanafunzi wenye talanta. Mara nyingi vipaji haviangaziwi wakati wa kuwaorodhesha wanafunzi ilhali wengine wao wanafanya vyema katika idara hiyo hadi kualikwa Ikulu kumtumbuiza rais,’’ alisema.

‘’Wengine pia hukosa kufanya vyema kutokana na mazingira yao ya kusomea. Kwa mfano, mwanafunzi anayesoma katika shule iliyoko sehemu zenye ukame kama Turkana si haki kumlinganisha moja kwa moja na yule anayesoma shule iliyoko kwenye miji kama Nairobi, Mombasa ama Kisumu,’’ alisisitiza Kamadi.

Kamadi vilevile anasema itakuwa haki kwa wanafunzi ikiwa shule zitaorodheshwa kwa viwango vya kitaifa, kaunti na wilaya, na wala sio kujumulisha kama ilivyokuwa ikifanyika hapo awali.

Bunge la taifa siku ya Jumanne lilipitisha mswada unaopendekeza utaratibu wa kuorodhesha shule uliopigwa marufuku na wizara wa elimu mwaka 2012 urejelewe wakati wa kutangaza matokeo ya mtihani wa kitaifa.

Mswada huo sasa unasubiri sahihi ya Rais Kenyatta kabla kuwa sheria na kuanza kutekelezwa.