Muungano wa walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri Kuppet, umetoa makataa ya siku saba kwa Waziri wa elimu Dkt Fred Matiang'i kufunga shule la sivyo washiriki mgomo.
Akihutubia waandishi wa habari huko Nairobi siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa muungano huo Omboko Milemba alisema Matiang'i anafaa kuagiza shule zifungwe ili kuitisha kikao na wadau wa sekta ya elimu kutatua suala la wanafunzi kuchoma shule.
“Tunachotaka ni waziri afunge shule zote nchini na wanafunzi waende nyumbani. Tuko tayari kumpa suluhu ya namna ya kusuluhisha mikasa hii ya moto iwapo atahitaji msaada wetu,” alisema Milemba.
Aidha, Milemba amepinga agizo la Tume ya TSC la kuwataka walimu wakuu na manaibu wao kulala shuleni, akisema kuwa linakwenda kinyume cha sheria za leba kwani walimu sio wataalamu wa masuala ya usalama na kuwa baadhi ya shule pia hazina nyumba za walimu.
Milemba vilevile alisema kuwa muungano huo utaiitisha mgomo wa walimu ikiwa Matiang'i hatoagiza kuachiliwa huru kwa walimu waliokamatwa katika baadhi ya shule zilichomwa kwa madai ya kuzembea au hata kushirikiana na wanafunzi kutekeleza uteketezaji huo.
“Siku saba zikikamilika kabla ya walimu wetu kuachiliwa huru basi hata wale wanaohudumu shuleni tutawaambia wakome kuenda,” alisema Milemba.
Wakati huo huo, wazazi waliozungumza na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Alhamisi waliunga mkono pendekezo la shule kufungwa wakisema ni wazazi ambao watagharamikia uharibifu unaotakana na mikasa hiyo.