Muungano wa walimu wa shule za upili na vyuo Kuppet umewahimiza walimu waliosahihisha mtihani mkuu uliopita kuwa na subira huku muungano huo ukifanya juhudi kuhakikisha kuwa wanapokea malipo yao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumatano, katibu mkuu wa Kuppet tawi la Mombasa, Lynnet Kamadi, alisema kuwa malipo hayo yamechelewa kutokana na mabadiliko yaliyotekelezwa na serikali katika uongozi wa Baraza Kuu la Mtihani nchini Knec.

‘’Tunawasihi walimu wetu wawe na utulivu pesa zao watapokea hivi karibuni. Kama siyo mageuzi yaliyotekelezwa katika baraza la Knec walimu wangekuwa washalipwa pesa zao,’’ alisema Kamadi.

Aidha Kamadi alisema kuwa katibu mkuu wa Kuppet Akelo Misori analishughulikia swala hilo na kuwa watatoa mwelekeo kabla juma hili kutamatika.

‘’Kwa muda sasa katibu wetu amekuwa na msururu wa mkutano na serikali na viongzoi wa muda wa Knec na tunamatumaini kuwa mwelekeo mwafaka utaoafikiwa wiki hii,’’ aliongeza afisa huyo wa elimu.

Haya yanajiri huku walimu walioutahini na kuusahihisha mtihani wa darasa la nane KCPE na kidato cha nne KCSE mwaka uliopita wakilalamika kutolipwa hadi sasa licha ya mkataba baina yao na Knec kueleza kuwa wanafaa kulipwa chini miezi mitatu baada ya kuusimamia mtihani huo.