Hatua ya serikali kuu ya kuwapunguzia viongozi idadi ya walinzi wanaandamana nao, inatekelezwa pasi na Wakenya kuelezewa sababu muhimu za hatua hiyo.
Afisa wa maswala ya haki za sheria katika Shirika la Utetezi wa haki za kibinadamu nchini Haki Afrika, Francis Auma Gamba, alisema kuwa jinsi mpango huo unavyotekelezwa unaonyesha uhasama wa kisiasa baina ya mirengo tofauti ya kisiasa nchini.
Auma alisema kuwa viongozi wana haki ya kupewa ulinzi kisheria, na mvutano wa hivi majuzi kati ya Serikali na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho unajenga fikra tofauti za kisiasa nchini.
“Tunaiomba serikali kulitatua swala hili vyema ili kuzuia kushughudiwa kwa uhasama wa kisiasa kwani hatua hiyo huenda ikaleta vurugu kutokana na baadhi ya viongozi kushikilia kutosalimisha salaha zao hata kuwa viongozi hao wanahitaji ulinzi,” alisema Auma siku ya Ijumaa mjini Mombasa.
Mwanaharakati huyo alishinikiza kuwe na mwafaka baina ya serikali na viongozi kuhusu suala hilo la kuwapunguzia walinzi, ili viongozi wasihisi kukandamizwa.