Kurutu mmoja alijipata matatani siku ya Jumatatu baada ya kudaiwa kuwa alikuwa mlevi alipokuwa akishiriki zoezi la uteuzi wa Makurutu katika Uga wa Michezo wa Gusii, Kaunti ya Kisii.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kijana huyo kwa jina Ben Nyakeri alitiwa pingu na kufungiwa ndani ya mojawapo ya gari la Polisi na baadaye kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kisii Central.

Kulingana na Afisa wa Polisi ambaye alimshika kijana huyo, Kurutu huyo alikuwa mlevi na alitaka kuleta vita na vurugu alipokuwa akichunguzwa katika harakati za kuteua Makurutu.

"Alikuwa amekunywa pombe maanake alikuwa na arufu ya pombe. Bila shaka ndio sabababu alikuwa msumbufu na kutaka kuleta vita hapa uwanjani,” alisema Afisa huyo wa Polisi.

Hata hivyo inadaiwa na baadhi ya walioshudia kitendo hicho kuwa kijana huyo alisusia kuzunguka raundi mbili zaidi kwenye uwanja kama wengine kwani aliwalaumu Maafisa hao kumlazimisha kuzunguka zaidi ya wengine wakati alishakuwa nambari wa pili kwenye mashindano na nafasi yake kupatiwa mwingine.

Kufuatia masaibu yote hayo kijana huyo alipoteza nafasi ya kuteuliwa na bahati yake nzuri inadaiwa kufikia mwisho wa zoezi hilo. Hata hivyo Kurutu huyo alikuwa ameachiliwa baadaye na kuonekana uwanjani Gusii akibeba baadhi ya vitu vyake alivyoacha humo uwanjani.

Hicho kilikuwa mojawapo ya visa ambavyo vilishuhudiwa katuka zoezi hilo la uteuzi kwenye Uga wa Michezo wa Gusii kwani hakukuwa na visa vingi ikilinganishwa na mwaka jana kama alivyodai msimamizi wa zoezi hilo Kamanda wa Polisi Fredrick Kagai.