Maafisa wa polisi walimtia mbaroni Kijana mmoja hapo jana wakati wa usajili wa makurutu wa kujiunga na idara ya polisi kwa kushutuma za udanganyifu katika zoezi hilo.
Zoezi hilo lililokuwa linafanyika katika uwanja wa michezo wa Gusii liliwaleta pamoja vijana kutoka maeneo bunge ya Kitutu Chache Kusini na lile la Nyaribari Chache.
Kijana huyo alitiwa mbaroni baada ya kubainika kuwa alitumia pikipiki katika zoezi la kukimbia kwa miguu na kutangulia wengine huku kudai kuwa ndiye aliyeibuka mshindi.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya jumatatu katika uwanja wa Gusii mjini Kisii, afisa aliyesimamia zoezi hilo Mohammed Kusolo alisema kijana huyo alitumia pikipiki na alionekana akishuka kutoka kwayo na kuanza kukimbia baada ya kutangulia wengine .
“Kijana huyu alitaka kutumia udanganyifu katika usajili huu na sasa tumemkamata kwa kosa la kutofuata sheria tulizoweka,” alisema Kusolo.
Kijana huyo alipelekwa katika kituo cha polisi mjini Kisii akisubiriwa kufikishwa mahakamani kushtakiwa.
Usajili huo ulifanyika kote nchini huku wengi wakikosa kufaulu kuchaguliwa kufuatia makosa madogomadogo.