Share news tips with us here at Hivisasa

Je, ushawahi kukutana na mwanamke ambaye amekolea katika ufundi wa magari kiasi cha kumfanya kwenda sambamba na wanaume katika kazi hiyo?

Na je, wewe unayemiliki gari utamruhusu mwanamke kulitengeneza gari lako linapokabiliwa na matatizo?

Kutana na Mourine Ondeyo, ambaye amekuwa akifanya kazi ya kutengeneza magari katika eneo la Jua Kali jijini Kisumu tangu mwaka wa 2009.

Ondeyo alifanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne KCSE, mwaka wa 2008 na kupata alama ya C+, katika Shule ya upili ya wasichana ya Ringa, Kaunti ya Homabay.

Ondeyo mwenye umri wa miaka 26 ni mzaliwa wa Oyugis, na ni mama wa mtoto mmoja wa kiume.

Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumatano katika karakana ya FM, anakofanya kazi, Ondeyo alisema kuwa alimua kufanya kazi ya kutengeneza magari ili kuudhibitishia ulimwengu kwamba wanawake wana uwezo wa kufanya kazi zinazoaminika kuwa za wanaume.

“Hii kazi nimeifanya tangu mwaka 2009 na kufikia sasa, hakuna kile nisichoweza kutengeneza kwenye gari,” alisema Ondeyo.

Alisema kuwa kazi hiyo humuwezesha kukidhi mahitaji yake ya kila siku, kumlipia mtoto wake karo na vile vile kumlipia dadake aliye kwenye shule ya upili karo.

Alitoa wito kwa Gavana wa Kisumu Jack Ranguma kuwajengea vibanda katika eneo la Jua kali, ili kurahisisha kazi yao.

“Mwaka jana, gavana alikuja hapa akaahidi kuwa atatujengea vibanda. Tunaomba kwamba ajengee hivyo vibanda kwa sababu kwa sasa tunafanyia kazi nje, na inakua vigumu kutekeleza majukumu yetu ipasavyo wakati wa mvua na jua,” alisema Ondeyo.