Mkurugenzi mkuu wa shule ya msingi ya kibinafsi ya Temudo jijini Kisumu Carmeline Tado, ameunga mkono agizo la waziri wa elimu Profesa Jacob Kaimenyi kwa walimu wakuu wa shule za umma dhidi ya kuwasajili wanafunzi kutoka shule za kibinafsi, mbele ya mitihani ya taifa.
Akizungumza hapo jana walipokuwa wakisherehekea matokea mazuri ya mtihani wa KCPE yaliyotolewa siku ya Jumatatu, Tado alisema kuwa kuna baadhi ya shule za umma zilizo na mazoea ya kuwaruhusu wanafunzi kutoka shule za kibinafsi, kusajiliwa katika shule za umma kama watahiniwa ili kuzifanya shule hizo kung’aa kwenye mitihani ya taifa.
Tado alidokeza kuwa sharti serikali iekeze katika sekta ya elimu, kwa kuimarisha miundo msingi, na kuongeza idadi ya walimu, ili kuboresha elimu nchini.
Kuhusu hatua ya wizara ya elimu kufutilia mbali mfumo wa kuorodhesha watahiniwa na shule kulingana na matokeo ya mtihani wa taifa, Mkurugenzi huyo alikuwa na hisia mseto.
“Nahisi kwamba ni jambo zuri kwa sababu wale waliokuwa na mazoea ya kushiriki katika wizi wa mtihani ili kuorodheshwa wa kwanza watakoma. Hata hivyo, hatua hiyo huenda ikasababisha wanafunzi kuzembea shuleni, kutokana na ukosefu wa ushindani,” akasema Tado.
Naye mwanafunzi bora wa kike katika shule hiyo ya Temudo Hafsa Shariff, aliyepata alama 404 amewashukuru walimu wake, kwa kumwezesha kufanya vizuri katika mtihani huo.