Ujenzi wa reli mpya kutoka mjini Mombasa hadi Nairobi ulianza rasmi baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu huku wadadisi wakisema kuwa mradi huo ni moja kati ya miradi mikubwa zaidi kuwahi kufanyika humu nchini.
Lakini kama ilivyo kawaida, kila mradi wa maendeleo unapotokea lalama za hapa na pale hazikosekani kutoka kwa wakaazi.
Katika mtaa wa Miritini, Kaunti ya Mombasa, wakaazi wa eneo hilo wanadai kuugua maradhi mbalimbali baada ya kampuni ya ujenzi wa reli kubomoa eneo lao la kufanyia tambiko na ibada za kitamaduni.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne, wakaazi hao walidai kuwa ubomozi wa sehemu hiyo ya ibada umeleta nuksi katika mtaa huo, huku wakiongeza kuwa hata wengine wao walifariki majuma kadhaa yaliyopita kutokana na hilo.
Mzee Abdalah Mohamed, mmoja wa wakaazi ambaye alidai kakake mdogo aliugua maradhi ya akili, alisema kwamba ubomozi huo ulifanywa kwa lazima bila kuwahusisha.
“Walikuja usiku na kubomoa eneo hilo. Baada ya hapo, tumekuwa hatuna tena sehemu ya kufanyia maombi na sasa tumeanza kuona watu wakiugua maradhi ya kiajabu,” alisema Mohamed.
Sehemu hiyo ambayo wenyeji wameipa jina Pindua Magongo imekuwa ikiheshimiwa sana na mtu anapougua, alikuwa akipelekwa hapo kwa matibabu ya kiasili.
Wazee wanadokeza kuwa watu wawili walifariki kutokana na magonjwa wanayoamini kuwa yalitokana na uharibifu huo, na kusema kuwa visa vya hivi karibuni ni watu kuugua macho na masikio na wengine kuchanganyikiwa kimawazo.
Hata hivyo, wazee hao walisema kuwa kampuni hiyo ya wachina imekataa kuwafidia kutokana na uharibifu wa makaburi ya eneo hilo, licha ya kuahidiwa kupewa fidia.
Wakaazi hao sasa wanaitaka kampuni hiyo kutimiza ahadi yake.
“Wakitupatia ile fidia walituahidi basi sisi tutaweza kufanya tambiko na kutoa sadaka kwa babu zetu ili watusamehe kutokana na masaibu yaliyotokea,” aliongeza mzee mwingine.