Hakuna jambo linalomfurahisha mwanamke kama kuchumbiwa na mwanamume ajuae kupika.
Kupika ni mojawapo wa ujuzi unaomfanya mwanamume awe wa kipekee.
Sio lazima kila siku mke ang’ang’ane na vyombo jikoni ilhali mumewe ameketi kwenye kiti kama kibonzo anatazama runinga ama kusoma gazeti.
Kumpikia mkeo ni ishara ya mapenzi. Upishi humpa mwanamume fursa ya kumwonyesha mkewe jinsi anavyompenda.
Katika ile hali ya kupika na mkeo, mtakuwa na nafasi mwafaka kuzungumzia mambo ambayo yatakuza ndoa yenu.
Kulingana na utafiti, kuna familia nyingi nchini ambazo mke na mume hukutana tu wakati wa kulala. Hili sio jambo nzuri kwa watu wanaotaka kuishi maisha ya furaha.
Ni vyema kutenga muda uwe na mkeo ili mjadiliane mambo kadhaa kuhusu ndoa yenu.
Mojawapo wa nyakati ambazo wapenzi wanaweza zungumzia maswala ya kifamilia ni wanapopika.
Mwanamume anayejua kupika ni mfano mzuri kwa wanawe. Watoto wakizaliwa na kumwona baba pia anapika watafahamu fike kwamba ndoa ni kusaidiana.
Kuna uwezekano mkubwa wa watoto hawa kuwa wenye hulka njema.
Sio wanawake wote wamelelewa wakipika. Mume aliye na ujuzi wa kuandaa aina tofuati ya vyakula atachukua fursa ya kumfunza mkewe.
Isitoshe, mojawapo wa ishara ya kumjali mkeo wakati mgumu kama vile anapogonjeka ni kuvuaa koti lako la Kitaliano kisha uelekee jikoni.
Kabla mpenzi wako hajalipa mahari, muulize ikiwa anajua kupika.