Maafisa wa kitengo cha kupambana na ugaidi mjini Mombasa walimtia nguvuni raia mmoja wa Marekani katika eneo la Nyali mjini Mombasa wakimshuku kuwa mshirika wa ugaidi.
Kamanda mkuu wa Polisi katika Ukanda wa Pwani Francis Wanjohi alisema kuwa raia huyo alinaswa na bastola mbili zikapatikana katika nyumba anayoishi pamoja na wanawake wawili.
Akizungumza na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Wanjohi alisema kwamba tayari uchunguzi wa kina umeidhinishwa kuhusiana na tukio hilo ili kubaini malengo ya raia huyo na shughuli ambazo alikuwa akifanya mjini Mombasa.
"Lazima usalama uimarishwe Pwani na magaidi watakabiliwa kikamilifi na maafisa wa polisi kwa sababu tuko na maafisa waliyohitimu na hakuna mtu ataleta vurugu na aachiliwe atakabiliwa kisheria na huyu gaidi atafikishwa mahakamani na sheria itachukuliwa sisi hatukubali ugaidi Pwani," alisema Wanjohi.
Wanjohi alisema kwamba kutiwa nguvuni kwa raia huyo kumetokana na habari muhimu ambazo kitengo hicho cha kupambana na ugaidi mjini Mombasa kimekusanya kutoka kwa wakaazi wa eneo hilo la Nyali na Mombasa kwa jumla wanaoishi karibu na nyumba ya raia huyo.
Wanjohi alisema kwamba raia huyo atafikishwa mahakamani punde tu maafisa wa kitengo hicho watakapokamilisha kumhoji mwanamume huyo wa umri wa makamu.
Hata hivyo, raia huyo wa Marekani alifikishwa mahakamani siku ya Jumatatu na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi nusu milioni pamoja na kuagizwa kuripoti katika makao makuu ya idara ya upelelezi mjini Mombasa kila mwisho wa mwezi kadri maafisa wa usalama wanavyoendeleza uchunguzi wao kuhusiana na kesi hiyo.