Kiwango cha ukuzaji mchele nchini kimeongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
Licha ya kiwango hicho kufikia tani 150, 000 kila mwaka, Kenya bado haijaafikia kiwango kinachotakikana cha tani 540, 000 kila mwaka.
Katibu katika wizara ya Kilimo Richard Lesiyampe alhamisi alisema kuwa uzalishaji wa mchele uliongezeka kutoka tani 50,000 mnamo mwaka wa 2008 hadi tani 149,661 mwaka 2015.
“Baadhi ya sera zinazoongoza sekta ya ukuzaji wa mpunga ni duni, na pamoja na kuingizwa hapa nchini kutoka mataifa ya nje mchele wa bei ya chini, zinafanya ukulima huu kutoongezeka kwa kasi,” alisema katibu Lesiyampe.
Lesiyampe aliyasema hayo baada ya kufungua rasmi mkutano wa kitaifa wa washika dau wa kilimo cha mpunga katika ukumbi wa mikutano wa shirika la utafiti wa kilimo na wanyama la KALRO mjini Naivasha.