Maafisa wa utawala mjini Nakuru Ijumaa asubuhi walinasa zaidi ya lita 5,000 za pombe haramu aina ya Kangara katika msako uliofanyika eneo la Mwariki, Nakuru magharibi.
Msako huo ulioongozwa na naibu kamishna eneo la Nakuru mashariki Elmi Shaffi pamoja na afisaa mkuu wa polisi wa utawala eneo hilo Barnabas Kimutai ulipelekea pia kuharibiwa kwa vyombo vinavyotumika kuendeshea shughuli hiyo.
Kulinganana na Shaffi ni kuwa mmiliki wa handaki hilo aliyetambulika kama Muriuki ni mmoja wa wapishi haramu ambaye ametajwa kumiliki kituo kingine mjini Nakuru kinachodaiwa kuuza pombe aina ya chang’aa kwenye chupa za pombe ambayo imeidhinishwa.
Shaffi aidha amewaonya wanaojihusisha na upishi haramu kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria huku akiapa kuendeleza zoezi hilo katika maeneo yote ya eneo hilo katika lengo la kusitisha upishi wa bidhaa hiyo haramu.
“Vita hivi nawahakikishia kuwa havitakoma hadi pale tutaona kuwa pombe haramu imemalizwa kabisa katika maeneo yote ya Nakuru na viunga vyake,” Shaffi alisema.
Wakati huo huo aliyataja baadhi ya maeneo yaliyoathirika na uhalifu pamoja na dawa za kulevya miongoni mwa vijana akiapa kuwa atahakikisha yamekwisha kwa ushirikano na machifu wa maeneo hayo na kuwahamasisha vijana hao kujihusisha na maswala ya kimaendeleo.
Zoezi sawia na hilo liliendelezwa katika eneo la London na kupelekea zaidi ya lita 3000 za pombe aina ya Kangara kunaswa hapo Alhamisi.