Maafisa wa zimamoto wa Kaunti ya Mombasa wamefanikiwa kuzima moto uliokuwa ukiteketeza lori la kuzoa taka karibu na uwanja wa manispaa ya Mombasa.
Kulingana na wakaazi walioshuhudia kisa hicho siku ya Jumatatu, moto huo ulizuka wafanyabiashara wa vyuma vikuukuu walipokuwa wakichoma tairi za gari karibu na lori hilo.
Wafanyabishara hao walilenga kunufaika na vyuma vya tairi hizo maarufu kama 'rim' lakini mambo yakageuka pale lori hilo lilliposhika moto na kuanza kuchomeka.
Hata hivyo, wazima moto wa kaunti walifika upesi na kudhibiti hali hiyo.
Hakuna aliyeripotiwa kujeruhiwa katika tukio hilo.