Chama cha mawakili nchini LSK, kimeshutumu maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kisiasa kuwakabili waandamanaji waliyokuwa wakishinikiza kubanduliwa kwa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne, Rais wa Chama hicho nchini Isaac Okero, alisema kwamba kipigo walichopokea wananchi hao kamwe hakikustahili.
Okero alisema kuwa wafuasi hao wa muungano wa Cord walifanya maandamano yao kwa amani, huku maafisa wa usalama wakiwakabili kwa marungu, makonde na mateke pasipo huruma yoyote.
Hata hivyo, Bwana Okero alisema kwamba maandamano hayo yalizongwa na uharibifu wa mali na wahusika wote wanapaswa kutiwa nguvuni na kushtakiwa mahakamani kwa kuharibu biashara za wenyewe.
Mwanasheria huyo aidha ameitaka serikali kuwaelimisha maafisa wa polisi kote nchini kuhusu katiba na haki za kibinadamu, ili kuzuia matukio kama hayo.
"Tunasikitishwa na hatua ya maafisa wa polisi kuwajeruhi wafuasi wa Cord wakati wa maandamano. Lazima serikali iwaelimishe maafisa hao kuhusu umuhimu wa kutangamana na Wakenya,” alisema Okaro
Chama hicho kinashinikiza majadiliano kati ya pande ya serikali na upinzani, ili kusuluhisha swala la IEBC ambalo kwa sasa limeonekana kuzua joto la kisiasa humu nchini.