Maoni mbali mbali yametolewa kuhusu aliyekuwa mama wa taifa Lucy Kibaki ambaye ameaga dunia akiwa anapokea matibabu katika hospitali moja mjini London.
Lucy atakumbukwa kuwa mama wa taifa ambaye amewahi mchapa kofi mwandishi wa habari ikuluni na ambaye alizungumziwa kuwa na visanga chungu nzima akiwa ikuluni.
Kulingana na Julius Mariita ambaye ni mmoja wa viongozi wa vijana katika kaunti ya Nyamira, atamkumbuka mama Lucy kuwa mama wa taifa ambaye alikosa heshima kwa wananchi na hata rais mwenyewe.
"Lucy alikuwa mkali sana, ata wakati mmoja alitoka kwa ndege mbele ya rais, jambo ambalo lilionyesha kuwa hakuwa anamheshimu hata rais Kibaki," alisema Mariita.
Hata hivyo, hakukosa mtetezi kwani Joan Omambia ambaye ni mfanyi biashara alimmiminia sifa chungu nzima akisema alikuwa mama mwenye msimamo.
"Lucy alikuwa mama wa bidii na ambaye alikuwa karibu na mzee wake sana kumsaidia kazi, hakupenda mchezo kwa kazi ndio maana alikuwa anaenda mikutano na rais Kibaki na hakuwa anapokea watu wenye hawana maana ikuluni," alisema Omambia.
Lucy Kibaki alikuwa mama wa taifa wa tatu nchini na ambaye atakumbukwa na wakenya kwa kuwa mstari wa mbele haswa kupigana na janga la ukimwi.