Bodi ya maabara nchini 'Kenya Medical Laboratory Technicians And Technologists' imewakamata watu wanne katika muda wa wiki moja iliyopita kwa kuendeleza oparesheni zao bila leseni.
Inspekta wa bodi hiyo Luka Chemwolo amesema jamaa hao walikamatwa baada ya uchunguzi kufanywa katika maabara 25 mjini Nakuru.
Chemwolo alisema kati ya maabara 25, ni maabara sita tu ambazo zilipatikana kufuatwa sheria za bodi hiyo.
Akiongea kwa njia ya simu siku ya Ijumaa, inspekta huyo alisema katika matukio mengine, maabara zilipatika kufuatwa sheria zilizopo lakini hata hivyo, zilipataikana na wahudumu ambao hawakuwa wamehitimu.
“Tumekuwa katika Kaunti ya Nakuru kuchunguza maabara kubaini iwapo sheria inafuatwa. Tulianza oparesheni hiyo siku ya Jumatatu na Jumanne tuliwakamata watu waliokuwa wakijifanya wahudumu wa maabara na tayari wamefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kuendeleza biashara ya maabara ilhali leseni zao zinawaruhusu kuendeleza famasia,” alisema Chemwolo.
Aliongeza, “Kufikia sasa, tumewakamata watu watano ambao hawakupatikana na leseni za kuendeleza maabara ambazo pia hazikuwa zimesajiliwa.”
Inspekta huyo alisema kwamba ilikuwa kinyume cha sheria kuendeleza uchunguzi katika maabara bila ya kukubaliwa na bodi hiyo.
Amedhibitisha kuwa bodi hiyo itaendela kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha sheria zimefuatwa.
Chemwolo alisema lengo lao mjini Nakuru halikufaulu kikamilifu kwa kuwa wamiliki wa maabara wamekuwa wakiwafahamisha wenzao kuhusiana na uwepo wa maafisa wao wanaoendeleza uchunguzi.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba licha ya hayo, hawatakoma kuendeleza uchunguzi wao akisema kwamba uchunguzi huo unalenga kufaidi umma.