Tume ya Hudumu kwa Polisi NPSC, imesema kuwa takriban maafisa wa polisi 300 kutoka kitengo cha trafiki watapigwa kalamu.
Hatua hiyo inajiri baada ya maafisa hao kushindwa kupeana stakabadhi za akaunti zao za benki pamoja na za Mpesa kwa tume hiyo ili kuwezesha ukaguzi dhidi yao.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Mombasa, Mwenyekiti wa tume hiyo Johnston Kavuludi alisema kuwa maafisa hao kutoka kanda ya Pwani pamoja na maeneo mengine nchini walipewa muda wa kutosha wa kutekeleza agizo hilo ila wameshindwa.
Maafisa hao walitakiwa kuwasilisha stakabadhi zao kufikia mwishoni mwa mwezi Machi ili kuwezesha zoezi hilo la ukaguzi litakalofanyika kati ya Mei 24 na Juni 4.
Zoezi hilo limelenga maafisa 598 kutoka Pwani, Magharibi na Nyanza katika awamu ya kwanza, na idadi ya maafisa 2500 kote nchini.