Serikali ya Kaunti ya Mombasa kupitia kwa Idara ya vijana, jinsia na michezo imeandaa hafla ya kuwatuza maafisa waliofuzu katika mafunzo ya lugha-ishara.
Maafisa hao wapatao 35 walipewa mafunzo hayo ya lugha-ishara kama njia moja ya kusaidia watu wanaoishi na ulemavu.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari baada ya hafla hiyo kukamilika siku ya Jumatano, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho alisema hatua hiyo itasaidia hutoaji wa huduma katika kaunti hasa kwa watu wanaoishi na ulemavu.
Mafunzo hayo yalihusisha maafisa kutoka katika vitengo mbalimbali ikiwemo afya, utalii, ofisi ya katibu wa kaunti miongoni mwa vitengo vingine.
Gavana Joho aliongeza kuwa wataendelea kutoa ufadhili ili maafisa hao waendelee na masomo zaidi.
“Serikali yangu hivi karibuni itawafadhili kwa miezi mingine misita ili kuongezea ujuzi zaidi katika maswala haya ya lugha za ishara,” alisema Joho.
Hatua hiyo ilipokelewa kwa furaha na baadhi ya wadau walioitaja kama njia moja ya kuwasaidia walemave ambao hukumbwa na changamoto ya mawasiliano kwa muda mrefu.
Hapo awali kundi la watu wanaoishi na ulemavu Mombasa lilijitokeza na kutaka serikali ya kaunti kuweka wataalam wa lugha-ishara katika ofisi za kaunti ili kurahisisha huduma.