Maafisa wa sekta ya afya katika kaunti ya Kisii wameifunga shule ya msingi ya Bomariba iliyoko eneo bunge la Bonchari kaunti ya kisii kwa kukosa vyoo vya usafi.
Wakizungumza na wanahabari siku ya Jumatano, maafisa hao, wakiongozwa na Isaac Getega waliamua kuifunga shule hiyo, baada ya maafisa hao kuipa shule hiyo siku 20 kujenga vyoo mpya na kukosa kufanya hivyo.
Shule hiyo imefungwa hadi wakati haujulikani, baada ya vyoo ambavyo vimekuwa vikitumika kuwa katika hali mbaya ambayo ingewafanya wanafunzi wengi kupata magonjwa mabaya, hayo ni kwa mujibu wa maafisa hao wa afya.
Naibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo Tom Nyamayo alisema shule hiyo iliandikia hazina ya CDF barua ya kuomba usaidizi wa pesa ambazo zingesaidia ujenzi huo, lakini hakuna jibu walilopokezwa kutoka hazina hiyo.
“Tuliandikia mbunge wetu Zebedeo Opore barua kupitia hazina ya ustawi maeneo bunge CDF ili watupatie pesa lakini hatukupatiwa jibu,” alisema Nyamayo.
Wakati huo huo, wakaazi wa eneo hilo ambao pia ni wazazi wa wanafunzi wa shule wamekashfu uongonzi wa mbunge wa eneo hilo kwa kutowajibiika ujenzi wa vyoo vya shule hiyo hiyo na kusababisha shule hiyo kufungwa.
“Sisi tunamlaumu mbunge wetu Zebedeo Opore kwa kutochukua hatua alipoandikiwa barua ya usaidi wa ujenzi wa vyoo, pesa za CDf anazipeleka wapi ? aluliza Zachary Nyambunde, mkaazi pia mzazi wa shule hiyo.