Maafisa wa afya kutoka Kaunti ya Kisii wamefunga Shule ya Msingi ya Gesere D.O.K iliyoko katika Wadi ya Ibeno, Kaunti ya Kisii kwa muda usiojulikana kufuatia kile walichokisema ni hali mbaya ya vyoo vya shule hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na Waandishi wa Habari mnamo siku ya Jumatano jioni, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Velster Onchari alisema Maafisa wa afya kutoka Kaunti ya Kisii walienda hadi shule hiyo na kuamrisha shule kufungwa hapo siku ya Jumanne kwa madai kwamba huenda wanafunzi waathirike na ugonjwa wa kipindupindu.

“Niliripoti katika shule hii mwezi wa pili mwaka 2010 na ifikapo mwezi wa tano, vyoo vya shule hii vikazama. Wazazi wa wanafunzi wa shule hii wakachanga pesa tukajenga vyoo vya muda ambavyo ni vya matope maana hatungeweza kujenga ya matafali kufuatia gharama vyao. Vyoo hivyo vya matope vimekuwa vikitumika hadi sasa,” alihoji Onchari.

“Maafisa wa afya walikuja hapa na kufunga shule wakisema wanafunzi wataathirika na ugonjwa wa kipindupindu iwapo wataendelea kutumia vyoo hivyo,” aliongezea Onchari.

Shule nyingi katika eneo la Kisii zimekuwa zikifungwa kutokana na hali ya vyoo ambavyo hulazimu Maafisa wa afya kufunga shule hizo.

“Tunaomba wasamaria wema kushiriakiana nasi ili tujenge vyoo vingine kwani wanafunzi wakiwa nyumbani kwa muda mrefu watapoteza muda wa kusoma,” aliomba Onchari.