Maafisa wa afya katika kaunti ya Kiambu Ijumaa walifika katika eneo la Kiandutu katika kaunti hiyo na kufunga vibanda vya kuuzia vyakula vya watu ambao hawakuwa na barua za idhini kutoka wizara ya afya.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu, huku watu kadhaa wakihofiwa kuhadhirika na ugonjwa huo, huku baadhi yao wakisemekana kulazwa katika hospitali ya Thika Medical wakionyesha ishara za ugonjwa huo.
Afisa wa afya katika mji wa Thika aliyeongoza operesheni hiyo aliwahimiza wakaazi wa eneo hilo kudumisha usafi nyumbani kwao, na pia waepuke kununua vyakula vinavyouzwa mitaani kwani ndivyo vinachangia ueneaji wa ugonjwa huo.
“Kipindupindu ni ugonjwa unaoua kwa haraka sana iwapo hatua mwafaka haichukuliwi, kwa hivyo, wale wanaouza vyakula, hakikisheni mmedumisha usafi wa maeneo ya kuuzia na vyombo vyenu,” alihoji Daktari James Njuguna, afisa wa afya eneo la Thika.
“Iwapo hatutaungana kumaliza maradhi haya eneo hili kwa mda ufaao, nahofia watu wengi, wakiwemo watoto watapoteza maisha yao,” aliongezea Njuguna.