Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Maafisa wa afya ya umma wameonywa dhidi ya kukagua nyama ya mifugo walioibiwa.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Itibo mifugo iliyokuwa imeibiwa ilipopatikana, Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga alisema kuwa amepata habari kuhusiana na maafisa wa afya ya umma wanaokagua nyama ya mifugo walioibwa kwa nia yakupewa hongo akiongezea kuwa uchunguzi unaendelea na huenda maafisa hao wakachukuliwa hatua kali ya kisheria.

"Kuna taarifa kuwa baadhi ya maafisa wa afya ya umma wanakagua kisha kuidhinisha uuzaji wa nyama ya mifugo walioibwa kwa minajili yakupewa hongo. Nawahakikishia kwamba pindi uchunguzi utakapo tamatika, maafisa husika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu," alisema Onunga.

Kamishna Onunga aidha alisema kuwa baadhi ya mifugo wa wizi huchinjwa majira ya usiku ili kuepuka kutambulika na kisha nyama kuuziwa wateja wasio na ufahamu wakati wa asubuhi.

Onunga aliwahimiza wananchi kuripoti mtu yeyote wanaye mshuku kuchinja mifugo wa wizi usiku.

"Nawahimiza wananchi kupitia kwa kundi lakudumisha usalama vijijini kupiga ripoti kwa maafisa wa polisi pindi wanapopata habari kuhusu mtu anayechinja mifugo usiku ili hatua kuchukuliwa dhidi ya wahusika," alisema Onunga.

Haya yanajiri baada ya wizi wa mifugo kukithiri kwenye mpaka wa kaunti ndogo ya Borabu na Bomet.