Maafisa wa afya ya umma katika kaunti ya Nyamira wamefanya msako mkali wa maeneo ya kuuzia vyakula na kufanikiwa kuwatia mbaroni zaidi ya wanabiashara kumi kwenye eneo la Kebirigo kwa kuendesha biashara zao katika mazingira chafu.
Kulingana na afisa aliyeongoza msako huo siku ya Jumanne, Andrew Ombati, kwa muda mrefu maafisa wa afya ya umma wamekuwa wakiwaonya wanabiashara wanaochuuza vyakula bila leseni, swala ambalo baadhi yao hulipuuza.
"Kwa muda sasa tumekuwa tukiwahimiza wachuuzi wa vyakula kama hivi wasio na lesini kufanya juhudi za kuwa na kibali hicho cha kuhudumu ila baadhi yao hupuuza swala ambalo limetulazimu kufanya msako huu wa dharura," alisema Ombati.
Afisa huyo wa afya aliongeza kusema kuwa waliotiwa mbaroni watafikishwa mahakamani hii leo, Jumatano, huku akiwahimiza wananchi kukoma kuchuuza vyakula mahala pachafu ili kuepusha maradhi yanayosababishwa na hali hiyo.
"Wale ambao tumewatia mbaroni leo hii watafikishwa mahakamani mapema Jumatano kujibu mashtaka ya kuhudumu bila leseni na kuendesha biashara zao kwenye mazingira chafu," alisema Ombati.
"Tunawaomba wachuuzi kuhakikusha kuwa wanatimiza masharti ili kuepusha maradhi yanayosababishwa na mazingira chafU," Aliongezea Ombati.
Aidha, aliongeza kuwa misako kama hiyo itaendelea katika sehemu kadhaa katika kaunti ya Nyamira, hadi pale maafisa wake watakapohakikisha kuwa vibanda vya kuuzia vyakula katika maeneo mengi eneo hilo vimo katika hali nzuri.
"Misako mingine kama hii itaendelea katika maeneo mengi kwenye kaunti hii hadi pale tutakapohakikisha kuwa maeneo yote yakuuzia vyakula yamo katika hali nzuri," alihoji Ombati.