Huku fujo kati ya wanafunzi wa Taasisi ya Gusii na Polisi likishika kasi siku ya Ijumaa, Maafisaa wa kutuliza ghasia almaarufu GSU, walipelekwa mjini Kisii ili kutuliza zogo hilo ambalo liliwalemea Askari wa kawaida.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanafunzi hao ambao walilalamikia kuuawa kwa wenzao Alhamisi na gari lililokuwa linaendeshwa na Afisa wa Polisi, walifunga barabara kuu ya Kisii-Keroka ambapo wenye magari walilazimika kutumia barabara mbadala za Coke, KARI pamoja na lile la Prisons ambazo zilisaidia kurahisisha usafiri.

Maafisa hao wa GSU baada ya muda walifanikiwa kudhibiti hali hiyo ambayo ilikuwa ikiendelea kuenea ambapo vijana wengi ambao wanashukiwa kuwa wa kuendesha Bodaboda na wale wa kuranda randa mtaani almaarufu Chokora waliendelea kupenyeza ghasia katikati ya mji wa Kisii.

Aidha Polisi hao hawakutaka kamwe uwepo wa Waandishi wa Habari yeyote kupiga picha wala kukaribia eneo la ajali hilo. Wakaazi wengi wa mji huo wamewalaumu Maafisa wa Polisi ambao walionekana kufyatua risasi ovyo kwa wanafunzi.

Kufikia Ijumaa jioni watu wanne waliripotiwa kupigwa risasi akiwemo dereva mmoja wa Matatu ambaye alipigwa risasi na kufa papo hapo.

Juhudi za Waandishi wa Habari kutaka kuzungumza na Afisa Mkuu wa Polisi katika Kituo cha Polisi Kisii Central hazikuzaa matunda kwani ilisemekana kuwa alikuwa anashughulikia fujo hizo za wanafunzi.