Spika wa bunge la kaunti ya Kisii Okerosi Ondieki amesema maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) hawakuhudhuria kesi iliyofikishwa mahakamani kuzuia uchaguzi kuandaliwa mwezi wa nane mwaka ujao.
Wawakilishi wadi watano wa kaunti ya Kisii walishtaki tume hiyo ya IEBC na kutaka uchaguzi wa mwaka 2017 kutoandaliwa mwezi wa nane kwa kile walichokisema kuwa itakuwa ni ukiukaji wa sheria kwani hawatakuwa wamemaliza miaka mitano afisini kulingana na katiba.
Wawakilishi hao walisema katiba inaeleza bayana kuwa uchaguzi unafaa kuandaliwa baada ya kila miaka mitano huku wakisema ikiwa uchaguzi huo utafanyika mwaka ujao itakuwa viongozi wamekaa afisini miaka minne jambo ambalo liliwalazimu kushtaki tume hiyo.
“Tume ya IEBC haikutuma maafisa wala wawakilishi wake na hatujui chanzo kwani walipokezwa habari hii ili kuhudhuria na kusikiza kesi hii,” alisema Ondieki.
Kesi hiyo itasikizwa tena mwezi Mei 2, 2016 katika mahakama ya Homabay.